Uchaguzi Kenya 2020: Je, chaguzi na siasa za Kenya ni somo kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki?

  • Rashid Abdallah
  • BBC Swahili
Raila na William Ruto

Ifikapo Agosti 9, 2022, Wakenya watashuka vituoni kwenda kuchagua wawakilishi wa nafasi mbali mbali, ikiwemo Wabunge, Maseneta, Magavana na kubwa zaidi ni kumchagua mrithi wa kukikalia kiti cha Rais wa sasa, Uhuru Kenyatta.

Atakaechaguliwa atakuwa rais wa tano wa taifa hilo tangu kupata uhuru Disemba 1963. Aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga na Naibu wa Rais katika serikali ya Kenyatta, bwana William Ruto, ndio wanaonekana kuchuana zaidi katika mbio za uraisi.

Hivi karibuni Ruto, kutoka chama cha United Democratic Alliance (UDA), alitangaza atakubaliana na matokeo yatakayo tangazwa na tume ya uchaguzi. Chama hicho pia kikamtaka Odinga wa Orange Democratic Movement (ODM) kuja na tangazo kama hilo.

Ni dalili kwamba mambo yanazidi kuiva kuelekea Agosti. Ila ni muhimu kwanza kuzidurusu siasa za Kenya, kwani mgombea kukubali kushindwa au kutokubali, historia inaonesha ndipo mzizi wa utulivu au vurugu katika siasa huanzia.

Siasa za mwongo mmoja na nusu:

Historia ya siasa za Kenya tangu kupata uhuru, hazijanusurika na matukio ya kutia doa demokrasia na uhuru wa kisiasa. Zipo nyakati za utawala wa mkono wa chuma, utawala wa chama kimoja na nyakati za vurugu na mauaji.

Miaka 15 nyuma, mauaji makubwa yalitokea katika uchaguzi wa 2007. Zaidi ya watu 1,000 waliuwawa na maelfu waliyakimbia makaazi yao. Yalikuwa ni mauwaji mabaya zaidi kupata kutokea katika chaguzi za Kenya huru.

Licha ya mwendazake Mwai Kibaki, aliyekuwa Rais kutoka 2002 hadi 2013 kumiminiwa sifa kedekede juu ya kukuwa kwa uchumi wa Kenya, ila vurugu za 2007/8 zimebaki kuwa kasoro kubwa katika uongozi wake.

Ulipofanyika uchaguzi mkuu mwaka 2013, haukuwa wa umwagaji damu. Utulivu na usalama ulitamalaki. Malalamiko makubwa yalitoka kwa kiongozi wa upinzani, Raila Odinga ambaye hakuridhishwa na matokeo ya uchaguzi, lakini nchi ikabaki kuwa salama.

Wahombea wenza wa Raila odinga na William Ruto

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Martha Karua na Roigathi Gachagua

Patashika ya kisiasa ilirudi tena katika uchaguzi wa 2017. Ripoti ya Tume ya Taifa ya Kutetea Haki za Binaadamu nchini Kenya (KNCHR), ilieleza kutokea uvunjifu wa haki za binaadamu, ripoti pia ikabainisha jumla ya watu 37 waliuwawa katika vurugu za uchaguzi.

Vuta nikuvute katika chaguzi za nchi jirani:

Kwa hakika nchi nyingi za Afrika Mashariki hazina historia nzuri katika chaguzi zake. Kabla ya Kenya kwenda kwenye uchaguzi, Tanzania ilifanya uchaguzi mkuu Oktoba 2020. Ripoti ya Shirika la kuteta Haki za Binaadamu (HRW), inaeleza juu mauaji ya watu 14 visiwani Zanzibar na vikosi vya usalama viki-elekezewa kidole kuhusika katika kadhia hiyo.

Kando ya hilo, Tanzania pia iliamua kuzima mitandao ya kijamii wakati wa uchaguzi, Jambo lililotatiza pakubwa uhuru wa watu kutoa maoni na kupata taarifa. Hili lilifanywa kwa hoja ya kuinusuru nchi na taarifa za uongo wakati uchaguzi ukiendelea.

Nchi ya Uganda ilifanya uchaguzi mkuu Januari 2021. Mwezi Novemba 2020, miezi michache kabla ya uchaguzi huo vikosi vya usalama vilitekeleza mauaji ya makumi ya wafuasi wa upinzani walioandamana katika jiji la Kampala, baada ya kiongozi wao Bobi Wine kukamatwa.

Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto 2013

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto 2013

Pia, Uganda ilishuhudia kuzimwa kwa huduma ya intaneti na mitandao ya kijamii. Vilevile, kulikuwa na ripoti za watu kukamatwa kiholela na kutoweka. Ripoti ya mwandishi wa BBC, Patience Atuhaire ya Machi 2021, ilieleza, mamia ya watu hawajulikani walipo.

Kipi kinatia moyo juu ya Kenya?

Kuna tofauti kubwa kati ya nchi ambayo hutafuta miafaka kila pakitokea vurugu za kisiasa, mfano nchi ya Kenya; na nchi ambayo hata zikitokea vurugu na mauaji hakuna meza ya mazungumzo kujadili namna ya kuboresha hali ya mambo, mfano Uganda.

Mauaji ya 2007 nchini Kenya, yalikuwa chachu kwa taifa hilo kutafuta katiba mpya ili kuondoa matatizo ya kisiasa. Katiba hiyo iliyoanza kufanya kazi 2010, imebaki kuwa msingi muhimu kwa maendeleo ya demokrasia nchini humo.

Baada ya vurugu za uchaguzi wa 2017, Rais Kenyatta na mpinzani wake Raila Odinga, walikaa meza moja kutafuta maelewano mwaka 2018. Ndipo hapo, ukapatikana ule msamiati maarufu nchini Kenya, "hand-shake."

Hayo yote yanaleta matumaini juu ya siasa za Kenya. Na ni somo kubwa kwa nchi jirani; kwamba milango ya mazungumzo ya kisiasa ni lazima kila wakati iwe wazi, ili kurekebisha na kusuluhisha mambo yaendapo kombo.

Ni vugumu kutabiri kipi kitatokea katika uchaguzi ujao, kwa kuzingatia historia ya vurugu zinazokuja na kuondoka; ila ni rahisi kusema kwamba lolote litakalotokea wanasiasa wa Kenya wameonesha historia nzuri ya kuwa tayari kukaa pamoja kutatua sintofahamu zao kwa manufaa ya Kenya na Wakenya.

Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga

Tangu uchaguzi wa Uganda umalizike na vurugu zitokee, hakuna kikao kati ya upinzani na utawala ili kujaribu kuweka mambo sawa kwa faida ya chaguzi zijazo. Bado mivutano inaendelea, na huenda ikaendelea hadi uchaguzi mwingine utakapofika.

Nchini Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan, anaonekana kujaribu mazungumzo na upinzani ili kuponya vidonda. Na pia, ameonesha dhamira ya kuboresha mifumo inayosimamia siasa za nchi hiyo. Ingawa mtangulizi wake hakuwa muumini wa mazungumzo ya kisiasa wala maboresho.

Rais anayeondoka madarakani, Uhuru Kenyatta, amedhihirisha uwezo mkubwa wa kuheshimu uhuru wa kisiasa nchini Kenya, serikali yake haijaendesha kampeni za kuandama upinzani au wale wanaomkosoa katika mitandao na vyombo vya habari.

Ni matumaini ya wengi; aina hiyo ya uongozi itadumu hadi siku za mwisho za uongozi wake, wakati Wakenya wakipiga kura. Kwa maneno mengine, wanasiasa na wafuasi wao watafanya shughuli za kisiasa bila kuingiliwa na dola.