Sheila Sheldon: Msichana wa miaka 9 mwenye kipaji kinachowashangaza wengi Mombasa Kenya

  • Abdalla Seif Dzungu
  • BBC Swahili
Sheila na picha ya rais Uhuru kenyatta

Chanzo cha picha, Sheila

Sheila Sheldon ana umri wa miaka 9 pekee lakini uchoraji wake ni wa kiwango cha juu ikilinganishwa na watoto wa rika lake.

Yeye huchora picha ili kujifurahisha lakini cha kushangaza ni kwamba licha ya kuanza uchoraji akiwa na umri wa miaka sita hajapata mafunzo yoyote ya uchoraji

Na tayari ameanza kugonga vichwa vya habari baada ya kuchora picha ya Rais Uhuru Kenyatta na kuvutia mwaliko katika ikulu ya rais huyo wa Kenya.

Vile vile amewahi kuchora picha za Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Gavana wa Kwale Salim Mvurya na mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir.

Kipaji cha uchoraji wake kwanza kiligunduliwa katika shule ya kimataifa ya Diani International School.

Sheilah na gavana wa Mombasa Hassan Joho akishikilia picha yake

Chanzo cha picha, Sheila

Maelezo ya picha, Vile vile amewahi kuchora picha za Gavana wa Mombasa Hassan Joho
Sheila akichora

Chanzo cha picha, Sheila

''Mimi uhisi vyema ninapochora'', anasema.

''Mara nyengine ninapokasirika huangalia kazi yangu na kufurahi''.

Mbali na uchoraji Msichana huyo ni Mwanamitindo, Mbunifu wa mitindo na mshairi.

''Nilipata msukumo wa kufanya kazi hii kutoka kwa rais wa Marekani Donald Trump-kwa sababu yeye hupenda watu kufanya kazi na kujisaidia''.

''Ninapochora mimi hufikiria sana familia yangu na vile tunavyoishi na lengo langu ni kuimarisha hali yetu ya Maisha''.

Tulipozuru nyumbani kwao katika eneo la Nyali mjini Mombasa, Sheila alikuwa akichora picha ya simba mkubwa mwenye rangi tofauti huku kando yake akiwa na watoto wa rika lake ambao alikuwa akiwafunza kuchora.

''Nachora simba huyu kwa kuwa ndiye mnyama ninayempenda kutokana na ujasiri wake na rangi hizi zinalenga kuwavutia watalii ama watu wengine kuhisi kutaka kumnunua wanapomuona'',alisema msichana huyo wa darasa la nne.

Sheila akichora picha ya simba

Chanzo cha picha, Sheila

Sheila akisimama na mmojawapo wa michoro yake

Chanzo cha picha, Sheila

Ndani ya nyumba hiyo kuna michoro mikubwa ya Wanyama, wanasesere na wanawake iliotundikwa ukutani.

''Mimi pia hupata fursa ya kuwafunza watoto wenzangu, kwa sababu unapokuwa na kipaji usiseme kwamba ni chako peke yako lazima uwafunze wengine'', alisema.

Nilivutiwa na idadi kubwa za picha za wanawake ambazo alikuwa amechora na nikataka kujua kwa nini anafanya hivyo.

'' Mimi huchora picha nyingi za wanawake kwa sababu ni watu wanaoteseka kama mamangu anateseka sana amefanyiwa upasuaji, hivyobasi mimi huwachora wanawake kwa sababu ni watu muhimu katika familia'',aliongezea

Anasema kwamba kipaji chake kinatoka kwa mungu na kwamba anataka kuwa mchoraji mkubwa wa wanasesere katika kampuni ya Disney nchini Marekani.

Mamake Sheila ambaye ni afisa wa Magereza anasema kwamba wamepata ufanisi mkubwa kimaisha tangu kipaji cha Sheila kigunduliwe.

Chanzo cha picha, Sheila

Lakini Sheila anapima vipi masomo yake na uchoraji? Tulipata fursa ya kuzungumza na mamake ambaye anasema kuwa kila mwanawe anaporudi nyumbani kutoka shule yeye hufanya kazi yake ya shule na baadaye kuanza kuchora.

''Sheila hawezi kukosa kuchora, na yeye uhakikisha kuwa anachora picha moja kwa siku kabla ya kulala''..

Mamake Sheila ambaye ni afisa wa Magereza anasema kwamba wamepata ufanisi mkubwa kimaisha tangu kipaji cha Sheila kigunduliwe.

''Tunashukuru kwamba tangu rais Uhuru Kenyatta alipomjua Sheila kupitia mchoro wa picha yake aliochora maisha yetu yamebadilika. Mimi nimepandishwa cheo kazini na mume wangu akipatiwa kazi ya kudumu katika halmashauri ya bandari nchini Kenya''.alisema.

Tulimuuliza kuhusu hisia zake za kwanza alipogundua kwamba mwanawe ana kipaji

''Kwa kweli mimi huwa siamini, humuona mwanangu kama mtu aliyebadilika, sijui hizi fikra za kuchora zinatoka wapi kwa sababu hakuna mtu anayeweza kuchora katika familia yetu, babake hawezi hata kuchora mguu'',anatabasamu na kucheka.

Sheila akionyesha picha aliyomkabidhi rais Uhuru kenyatta

Chanzo cha picha, Sheila

Shuleni mwalimu wake Sheila Quinta Ndeche anasema kuwa ni mwanafunzi mwenye tabia tofauti ikilinganishwa na wanafunzi wenzake na ni mtu anayejituma .

Anasema kuwa ni mwanafunzi mtulivu anayepanda masomo yake na wakati wa kufanya kazi zake .

Mwalimu quinta anaongozea kwa kusema kwamba shule hiyo hujaribu kukuza kipaji chake kupitia kufanya kikao mara kwa mara na mwalimu wa Sanaa.